Matumizi Ya Sadfa Katika Riwaya Pendwa Ya Kiswahili: Mifano Kutoka Kivuli, Kikosi Cha Kisasi Na Hofu

IKISIRI

Tasinifu hii ilijikita katika kujadili matumizi ya sadfa katika riwaya pendwa za Kiswahili. Sadfa ni hali ya utukiaji wa matukio kwa wakati mmoja, aghalabu kwa namna inayoshangaza au inayoashiria bahati (Wamitila, 2003). Utumiaji wa mbinu hii katika kuibua matukio husababisha riwaya, hususani riwaya pendwa, kuonekana kuwa na matukio yasiyokuwa na mantiki katika utokeaji wake. Utafiti huu ulifanyika ili kubainisha athari za matumizi ya sadfa katika riwaya pendwa kwa kuchunguza vijenzi na miktadha ya utokeaji wake katika riwaya. Riwaya teule zilizotumika kuchunguza athari za matumizi ya sadfa ni Kivuli, Hofu na Kikosi cha Kisasi. Data zilikusanywa kwa njia ya uchanganuzi matini na usaili kwa wataalamu wa fasihi. Maeneo yaliyohusika kukusanyia data ni Dodoma na Dar es Salaam. Mbinu ya usimulizi ndio iliyotumika katika uchanganuzi wa data kwa kuzingatia misingi ya nadharia ya Umuundo. Matokeo yanaonesha kuwa kuna matumizi makubwa ya sadfa katika riwaya pendwa za Kiswahili na tanzu nyingine za fasihi. Yanabainisha mandhari, mwonekano, kazi, ushujaa na muundo wa wahusika kuwa ni vijenzi vinavyochagiza kuwepo kwa sadfa katika riwaya. Aidha, matokeo yanabainisha miktadha kama: mapenzi, upelelezi, safari, hali ya kukata tamaa na kushangaza kuwa inajengwa zaidi na sadfa katika kukamilisha masimulizi. Vilevile, athari zitokanazo na matumizi ya sadfa ni: kukuza taharuki, kupeleka matukio mbele (haraka zaidi), kuwakutanisha wahusika, kuburudisha na kijenzi cha unusura. Upekee wa tasinifu hii unatokana na kuongeza mawanda ya kuzitazama riwaya pendwa kwa jicho la sadfa ili kubainisha muundo na mtindo wake. Pia, kuondoa mtazamo hasi juu ya ujenzi wa matukio katika riwaya pendwa (mtazamo unaoamini kuwa matukio ya riwaya pendwa yamejengwa katika hali isiyokuwa na mantiki). Utumikaji mzuri wa mbinu ya sadfa hufanya kazi za fasihi kuaminika kwa urahisi zaidi na hadhira lengwa.