Usawiri Wa Mwanamke Katika Muziki Wa Nyimbo Za Dansi: Mifano Kutoka Katika Nyimbo Za Mbaraka Mwinshehe

IKISIRI

Utafiti huu ulijadili kuhusu Taswira ya mwanamke katika Muziki wa Nyimbo za Dansi teule za Mbaraka Mwinshehe. Tatizo lililojenga utafiti huu ni kutokana na hali ya kila siku iliyopo kwa wasanii wa muziki wa nyimbo za dansi, wakiwemo wanaume, kumkweza mwanaume kinafasi na kimajukumu na kumtweza mwanamke.

Utafiti ulitumia mbinu ya maktabani kwa kuchunguza kazi mbalimbali zilizoandikwa kuhusu usawiri wa mwanamke na mgawanyo wa majukumu kijinsia. Pia, nyimbo teule za Mbaraka Mwinshehe zimesikilizwa kwa makini ili kuweza kujua ni jinsi gani mwanamke amechorwa. Pia, mahojiano yalifanyika ili kuweza kupata na kuelewa kwa undani mada ya utafiti. Nadharia iliyoongoza utafiti huu ni ya Ufeministi, hususani wa Kiafrika, ambao una mawazo yanayozungumzia harakati za kumkomboa mwanamke katika jamii inayomdharau na kumkandamiza. Utafiti umebaini kuwa kuna tofauti kubwa za kimajukumu kati ya mwanamume na mwanamke katika jamii. Kwa asilimia kubwa, mwanamke amechorwa kwa upande hasi, yaani mnyonge, tegemezi na kiumbe duni. Hali imefanya mwanamke azidi kudharaulika, kutothaminiwa na kukejeliwa. Kwa kiasi kidogo, amechorwa ni mtu muhimu katika familia, hususani katika suala la kumstarehesha mwanaume awapo na shida. Vile vile, utafiti umebaini kuwa kuna athari kubwa kwa jamii zinazosababishwa na usawiri wa mwanamke katika nyimbo za dansi. Athari mojawapo ni kwa wasomaji kuiga matendo mabaya ambacho ni chanzo cha mwanamke kuendelea kudharaulika na kutothaminika katika jamii. Athari